Friday, April 16, 2010

FALSAFA ZA SENSEI SHIGERU EGAMI KUHUSIANA NA MAFUNZO YA SANAA ZA MAPIGANO

Huko China, magombo mwawili marufu kuhusu sanaa za mapigano ni Ekkin Gyo na Ekkin Zenkui.
Wanazuoni wengi wanaamini kwamba Daruma(Bodhi Dharma) ndiye aliye viandika vitabu hivyo katika
hekalu la Shaolin. Magombo haya yanaeleza ni kwa namna gani mtu anatakiwa kujifunza huku akiitakasa
nafsi yake.

Inaaminiwa kwamba Karate-do ilizaliwa kutoka kwenye mtazamo huu.

Kwa mafunzo na mazoezi, matatizo hupata suluhu.

Adui wa kwanza ni nafsi yako!

Lengo kuu la Karate-Do ni kupigania mwenendo sahihi wa tabia(kupigania tabia njema).

Ukijaribu kuyapunguza madhaifu yako katika kila siku ya maisha yako.

Ni nini maana ya upatanisho? Ni nini maana ya maisha? Amani ni nini? Umoja ni nini?

Natamani kuelewa uhusiano baina ya watu, baina ya watu na uasili wa mazingira yao.

Mwili na roho ni kitu kimoja.

Uimarishwaji wa mwili hukuza akili. Mwili uliozorota huzorotesha akili. Hiyo ndiyo sababu kuu iliyo
msukuma Daruma(Bodhi Dharma) kuanzisha mafunzo ya sanaa za mapigano katika hekalu la Shaolin takriban
miaka 1500 iliyopita.

Ni kwa mazoezi ndipo utapomudu ustadi wa mbinu. Lakini kamwe lengo la jitihada zako halitakiwi liwe
ni kujionyesha au Kupoteza amani.

Kutokana na uasili wa binadamu, ni vigumu mno akaishi peke yake. Binadamu anahitaji utulivu wa nafsi
lakini wakati huohuo anawajibika kuwapa amani wale wanaomzunguka. Atatakiwa awatendee wengine kama
ambavyo yeye angependa kutendewa. Unajaribu kuwaelewa wengine kwa kuielewa nafsi yako kwanza.

Hii ndio njia ya mafunzo. Natumaini wote tutajifunza huku tukizikagua nafsi zetu katika kupigania
mwenendo sahihi wa tabia.

Saturday, April 10, 2010

"K 3" ZA KARATE

Kumite ni moja ya tawi la karate ambalo huwavutia sana watu wanaoanza mafunzo ya karate, na hata
watu wanaopenda sanaa za mapigano kwa ujumla wake. Zaidi ya asilimia sabini ya wanafunzi wanaoanza
mafunzo ya karate hutaka kufundishwa namna ya kupigana haraka iwezekanavyo. Na hii ni moja ya
sababu kuu zinazo sababisha mbinu za msingi (kihon) kufanywa kwa uchache sana na pasipo uangalifu.

Hata mimi binafsi nilifurahi nilipokua napewa fursa ya kushiriki kwenye kumite, na nikawaida kwa
mwanafunzi yeyote aliye kwenye mikanda ya awali. Hivyo ni jukumu la mwalimu kuhakikisha kwamba
"K" tatu za karate (kihon, kata na kumite) zinafanywa kiusahihi na kwa uwiano sahihi ili kuepusha
wanafunzi kuelemea upande mmoja na kusahau "K" nyingine, kwani hizo "K" tatu ni kama magurudumu ya
bajaji nikiwa namaanisha hakuna inayopaswa kuachwa.

Kuna wanafunzi wanaodhani kwamba baada ya kujua namna ya kujihami au kumite basi tayari wanakuwa
wameishajua kila kitu kuhusiana na karate. Na kuna baadhi yao hupunguza hata mahudhurio katika dojo.
Haya ni makosa makubwa sana kwenye karate.

Ijapokuwa tunasisitiza mwanafunzi kufundishwa "K" tatu kwa usahihi lakini kiufundi "kata" na "kihon"
ni zakutiliwa mkazo zaidi katika mafunzo. Hiyo haimaanishi tuisahau kumite, la hasha. Mara nyingi
walimu wataalamu na wenye uzoefu huweza kuangalia "kata" ya mwanafunzi na kuweza kuainisha ikiwa
ni pamoja na kujua "kihon" au "kumite" yake itakuwaje. Lakini inaweza kuwawia vigumu kupata uelewa
wa "kata" na "kihon" ya mwanafunzi kwa kuangalia "kumite" yake. Na walimu wakubwa wengi hupenda
kujaji uwezo wa karateka kwa kuangalia "kata". Kata ni kipimo rahisi kuliko vyote katika kutambua
kiwango cha karateka. Kata mbovu, moja kwa moja huashiria kiwango kibovu na ufinyu wa taaluma.
Hakuna uvungu wa kujificha katika "kata".

Hii mada ni ndefu sana na inaweza kutoa maswali mengi haswa kwa wapenda "kupigana" lakini kwa leo
wacha niishie hapa.