Friday, January 15, 2010

BAADHI YA SABABU ZA STAILI NYINGI ZA KARATE KUCHEZWA PEKU(PASIPO VIATU)

i)Utamaduni wa wajapani.
Wajapani huvua viatu kabla ya kuingia kwenye nyumba zao. Hivyo basi kutokana na kwamba
karate imechukua sehemu kubwa sana ya utamaduni wa wajapani, kuvua viatu kabla ya
mafunzo ni itifaki mojawapo inayopaswa kuzingatiwa. Baadhi ya itifaki nyingine ni kusalimia
au kutoa heshima kwa kuinamisha kichwa, kutamka mbinu za karate kwa lugha ya kijapani n.k.

ii)Kuimarisha miguu.
Hii ni pamoja na kuongeza usugu na unene wa ngozi ya mguu.

iii)Kupunguza eneo la sehemu ya mguu inayoshambulia.
Kwenye fizikia imedhihirishwa kwamba mgandamizo huongezeka kutokana na kupungua kwa
eneo
. Hivyo basi ili kuongeza madhara ya shambulizi katika shabaha au eneo lililokusudiwa, ni
vyema eneo la kushambulia likapunguzwa kadri iwezekanavyo.

iv)Msafirisho wa nishati(ki) kutoka ardhini.
Mgusano baina ya unyayo na ardhi hurahisisha usafirishaji wa nishati isiyoelezeka kwa urahisi kutoka
ardhini na kuingia kwenye mwili. Ukufunzi wangu hautoshi katika kulielezea jambo hili.

KIHON NI NINI?
Kihon ni neno la kijapani linalo maanisha mbinu za msingi. Hii ni pamoja na upigaji wa ngumi au teke,
namna ya kupangua ngumi au teke, matumizi ya sehemu mbalimbali za mwili katika ushambuliaji.

SENPAI au SEMPAI NI NANI ?
Senpai ni neno la kijapani lenye maana ya mtu anaye simamia mafunzo ya karate kwa niaba ya Sensei.
Sen’ maana yake ni ‘kabla’ kama ilivyo kwa Sensei na ‘pai’ maana yake ni ‘kundi’. Hivyo senpai ni mtu
anayesimamia kundi fulani kutokana na kwamba ni mjuzi wa maarifa kuliko walio wengi katika kundi.

Saturday, January 9, 2010

MUHTASARI WA MASHINDANO YA KATA ITALY



MAANA YA KATA KATIKA KARATE
Kata ni makabiliano ya kufikirika baina ya karateka na wapinzani kutoka pande mbalimbali.
Tunatumia neno wapinzani badala ya maadui kwa sababu kwenye falsafa za karate hatuna adui.
Kila staili ya karate ina kata zake ijapokuwa baadhi zinafanana kiustadi, majina n.k.

Vipengele vitatu muhimu ambavyo karateka anapaswa kuvizingatia pindi aichezapo kata:
i)Nidhamu katika matumizi ya nguvu. Nguvu kuu inapaswa kutumika katika ile sekunde
ya shambulizi tu, baada ya shambulizi karateka atatakiwa kutoka katika hali ya ukakamavu
ili kuepuka uzalishaji wa nguvu isiyo na matumizi na hatimaye kupoteza nguvu bila sababu.
Lakini kuna kata kama hangetsu au kata nyingi za gojyu-ryu ambazo humtaka karateka
kukakamaa kuanzia mwanzo wa kata mpaka mwisho. Hapo kipengele cha kwanza si lazima
kipewe kipaumbele.
ii)Udhibiti wa spidi ya mbinu. Karateka anapaswa kutambua vyema ni mbinu gani katika kata
zinapaswa kufanywa taratibu na zipi atatakiwa kuzifanya haraka iwezekanavyo, hii pia hutumika
katika kuijua spidi ya karateka. Kama ilivyo kwa mwanamichezo au msanii, karateka anatakiwa
audhibiti mwili wake na si mwili umdhibiti yeye.
iii)Mikao na hatua sahihi pamoja na upumuaji.
Mikao na hatua katika kata ni lazima viwe sahihi ili kutoa tafsiri sahihi ya kata. Lakini pia namna
ya upumuaji ni kitu muhimu mno hasa katika viwango vya juu sana kwenye karate. Kuna wakati
upumuaji hupewa kipaumbele kuliko mbinu ya karate kwa sababu pumzi ni uhai. Upumuaji
mzuri utamsaidia sana karateka katika matumizi ya nguvu na kumfanya aweze kudumu kwenye
zoezi au pambano kwa muda mrefu.

Hivyo ni vipengele muhimu sana katika kata, vipengele vingine muhimu ni kama ; uzatiti wa wazo katika mbinu, mtikiso wa kiuno, kutanuka na kusinyaa kwa mwili na hatua, uelekeo, mlio wa shambulizi(kiai ), nidhamu, shabaha ya mbinu, stemina, muda, kujiamini, morali, tahadhari (zashin) na kadhalika.

Friday, January 8, 2010

SENSEI NI NANI ?
Huko Japani kila mwalimu huitwa Sensei. Lakini pia mwanasheria au daktari huitwa Sensei kutokana na
kwamba ni msomi au mjuzi wa maarifa kuliko walio wengi.Pia kama ilivyo ada kwamba wanasheria wengi hujihusisha na maswala ya siasa hivyo huko Japani kunawakati mwanasiasa pia huitwa Sensei .

Lakini labda wengi wamewahi kujiuliza kwamba ni sifa zipi hasa zinazomfanya mtu awe Sensei?
Watu wanaoitwa Sensei wanatakiwa kuishi kama walimu katika maisha yao yote.
Kimsingi neno Sensei limetokana na maneno mawili ya kijapani yaani ‘sen’ na ‘sei’.
i) ’sen’ maana yake ni kabla.
ii)’sei’ maana yake ni kuzaliwa.
Hivyo Sensei ni mtu ambaye amezaliwa kabla(kifikra) au mtu aliyepata ujuzi wa jambo fulani kabla ya
wengine. Heshima ni moja ya vigezo vikubwa sana kwa mtu anayeitwa Sensei.
Anatakiwa kuheshimu kila kiumbe chenye uhai. Hii ni kwa sababu heshima ni kitu muhimu sana
katika kujenga uhusiano mzuri miongoni mwa viumbe hai akiwemo binadamu.

Mara nyingi kwenye karate cheo cha usensei hutolewa katika mazingira yafuatayo :-
1)Karateka aliye kwenye daraja la mkanda mweusi na ana wanafunzi ambao yeye kama mwalimu
huwafundisha na kuyaishi yale anayoyafundisha. Huyu anapaswa kuitwa Sensei haswa na wanafunzi
wake. Si lazima kuitwa Sensei na kila karateka ila wanafunzi wake.
2)Karateka aliye kwenye daraja la mkanda mweusi na aliyeteuliwa na shirikisho fulani la kitaifa
au kimataifa kuwa Sensei. Huyu kwa heshima na taadhima anapaswa kutambuliwa kama
Sensei na karateka yeyote.

Saturday, January 2, 2010

MAANA YA KARATE

Neno karate ni muunganiko wa maneno mawili ya kijapani, yaani ‘kara’ na ‘te’.
1. ‘kara’ inamaanisha au kuelezea
(a)Pasipo silaha.
(b)Fikra iliyo huru(tupu) na yenye kuakisi
mazingira yanayoizunguka bila
kubugudhiwa.
2. ’te’ inamaanisha mikono.
Hivyo basi karate kama neno moja ni ‘mikono mitupu’ ikiwa na maana ya kujihami pasipo
matumizi ya silaha.
Kimsingi karate ni sanaa inayoendelezwa kupitia mila ,desturi na tamaduni mbalimbali ikiwa
na malengo yafuatayo:-
(a) Kumuwezesha msanii wake kuweza kujihami katika mazingira hatarishi bila kujali
umri, nguvu, umbo au jinsia aliyonayo.
(b)Kumpa karateka(msanii wa karate) afya njema iliyo imara.
(c)Na kubwa kuliko yote, kupigania mwenendo sahihi wa tabia. Hili ndilo lengo kuu la karate.

HISTORIA YA KARATE KWA UFUPI

Kutoka kwenye mchoro ufuatao :-




NAMNA KARATE ILIVYO STAWI

Takriban miaka mia sita iliyopita, mfalme Sho-Hashi wa Okinawa alianzisha sera iliyopiga
marufuku umiliki wa silaha katika visiwa vya Okinawa.
Mnamo mwaka 1609, silaha zote zilitaifishwa na serikali ya Okinawa. Hiyo ikapelekea watu
wengi wa Okinawa kujifunza mbinu za kujihami pasipo kutumia silaha, ndipo karate ilipo melea.
Hivi leo karate inaendelea kustawi kutokana na faida mbalimbali ambazo watu wanatarajia
kuzichuma kutoka kwenye sanaa hiyo ikiwa ni pamoja na muongozo wa kiroho au tabia,
sababu za kiuchumi,mbinu za kujihami n.k.

BAADHI YA FAIDA ZA KARATE

•KUPIGANIA MWENENDO SAHIHI WA TABIA
Lengo kuu la karate si ushindi dhidi ya mpinzani au jambo fulani bali ni ushindi
dhidi ya nafsi yako mwenyewe. Hii ndio karate-do. Neno ‘do’ lina maana ya ‘njia’.
Sote tunajua kwamba hakuna mtu kati yetu aliye mkamilifu hivyo basi ni vema
kila mmoja wetu akajitahidi kupunguza madhaifu yake katika safari ya maisha
yake. Hii ndio njia ya karate yaani ‘ karate-do’.
Madhaifu yanayoelezwa hapa ni kama hasira kali, uzinzi, ulevi, aibu iliyokithiri
au kutokujiamini, woga, uvivu, tamaa, husuda, chuki, kujisikia, dharau, majungu n.k.
Ni vema ikaeleweka kwamba sanaa haimjengi mtu bali mtu ndiye
huijenga sanaa ikiwa na maana ya kuifanya karate kuwa sanaa bora na muhimu
katika maisha yetu tofauti kabisa na ambavyo imekuwa ikichukuliwa.
Lakini kamwe karate haitoweza kumsaidia mtu kitabia mpaka pale atakapo pata
mafunzo kutoka kwa mwalimu ambaye ni msomi na mtaalamu wa sanaa hiyo.
Wataalamu na wasomi wa karate wapo wachache mno na walimu wengi si wataalamu
hivyo ni vema kuwa makini mara mtu atafutapo shule ya kujifunza kwasababu ni
vigumu mno kupima utaalamu na elimu ya mwalimu.

•UWEZO WA KUJIHAMI PASIPO KUHITAJI SILAHA
Kama ndege, wanyama na mimea mbalimbali ina namna au mbinu za kujihami
kwanini asiwe binadamu ?!.

Karate inamuwezesha karateka kuweza kujihami katika mazingira hatarishi
pasipo kujali umri, jinsia,nguvu au umbo alilonalo. Itagharimu nguvu ndogo sana
pamoja na ustadi sahihi wa mbinu ya karate katika kuimudu hali ya hatari.

•NIDHAMU NA KUJITAMBUA KATIKA MAZINGIRA MBALIMBALI
Karateka ni lazima muda wote awe mwenye nidhamu, aitambue nafsi yake
pamoja na mazingira yanayomzunguka. Hii itamuwezesha kutimiza wajibu wake pale
atakapo hitajika kufanya hivyo. Lakini pia karateka kama mtu yoyote atakuwa
na marafiki wenye tabia mbalimbali hivyo kuna wakati atatakiwa kuheshimu
maamuzi na mitazamo yao pindi watakapo kuwa pamoja. Hii kwenye karate
tunaita ‘ roho yenye muafaka ‘.

•AFYA NJEMA ILIYO IMARA
Karate inamsaidia karateka katika kuimarisha afya yake kupitia mazoezi na taratibu
mbalimbali zilizopo mafunzoni. Waweza kuitumia karate katika kupunguza uzito
wa mwili, kujenga misuli yenye nguvu, kujenga mifupa na viungo imara n.k.

•MTU YEYOTE ANAWEZA KUJIFUNZA KARATE
Tofauti na sanaa nyingi za mapigano, karate haimbagui mtu katika mafunzo yake.
Pasipo kujali jinsia, umri, nguvu au umbo; mtu yeyote anaweza kuanza mafunzo
ya karate hata kama ana umri wa miaka hamsini(50) na kuendelea alimradi
atakuwa akifundishwa na mwalimu mtaalamu na msomi wa karate ambaye ataweza
kutofautisha mafunzo kulingana na umri, jinsia, nguvu na umbo la mwanafunzi.

BAADHI YA MATATIZO YANAYOIKUMBA KARATE YA TANZANIA

•UTAALAMU WA WALIMU WA KARATE
Walimu wengi hapa nchini hawana taaluma ya kutosha kuhusiana na karate, hiyo inapelekea
kutoa mafunzo yasiyo sahihi na hatimaye kutoa picha potofu juu ya sanaa hii.
Hii ni pamoja na jamii kudhani kwamba karate ni swala la ngumi na mateke tu au ni sanaa
inayoweza kufundishwa kwa jinsia fulani au umri fulani tu. Wengine hugubikwa na
hofu ya kuvunjika viungo, kupiga watu hovyo, kuwa jambazi, kupoteza maisha n.k.
Karate ni sanaa nzuri sana kama ikifundishwa kwa usahihi lakini ni sanaa mbaya mno
na hatari kama itafundishwa na mwalimu asiye na taaluma ya kutosha kuhusu karate.


•HALI NGUMU YA KIUCHUMI
Mitihani ya kimataifa ya madaraja ya karate ni gharama mno ukilinganisha na hali ya
kiuchumi ya makarateka wengi wa Tanzania.
Gharama ya kila mtihani wa kimataifa wa madaraja ya mkanda mweusi si chini ya dola 100 za
kimarekani. Tanzania ina walimu wachache mno wenye mamlaka ya kutahini japo daraja la
kwanza la mkanda mweusi, hiyo inapelekea watu kufikiria aidha kumleta mwalimu kutoka nje
ya nchi ikiwa ni pamoja na kugharamia tiketi ya ndege(kuja na kurudi), mahali
atakapo fikia, usafiri n.k au mtahiniwa kwenda nje ya nchi ili kutahiniwa.

•MAZINGIRA YA KUFUNDISHIA KARATE
Ijapokuwa karate haibugudhiwi sana na ukubwa wa eneo la mafunzo tofauti na sanaa au
michezo mingine lakini karate ni lazima ifundishwe kwenye sakafu nyororo isiyo na muinuko.
Vilevile mahali pakufundishia karate ni vema pakafunikwa au kuzungushiwa uzio ili kuondoa
mazingira ya wanafunzi kubugudhiwa na watu wataoamua kutazama mafunzo ya karate.
Tanzania ina shule chache mno za karate zinazo zingatia viwango vya kimataifa .

•UTAPELI
Kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa mstari wa mbele na hata kujitangaza kwenye
vyombo vya habari kwamba ni waalimu wakubwa wa sanaa ya karate pasipo na utaalamu
wa sanaa hiyo. Wengine huangalia video za sanaa mbalimbali za mapigano na kuzitumia
video hizo kama nyenzo za kufundishia, wakati wengine hutoa historia za uongo kuhusu
hatua mbalimbali walizopitia katika kujifunza sanaa hii ikiwa ni pamoja na kutaja majina
ya walimu maarufu wa karate duniani.
Mara nyingi watu wa namna hii hutumia kujiamini kwao ili kumshawishi mwanafunzi
kwamba ni walimu wakubwa wa sanaa hii ya mapigano. Hivyo basi ni vema mtu ambaye
anataka kujifunza sanaa hii akafanya utafiti wa kutosha ijapokuwa ni ngumu ili kupata
mwalimu mtaalamu na msomi atakayeweza kutoa mafunzo sahihi.

•ELIMU DUNI/POTOFU KATIKA JAMII YA KITANZANIA KUHUSIANA NA KARATE
Karate imekuwa ikichukuliwa kama sanaa hatari na isiyofaa kundishwa katika jamii
mbalimbali. Mitazamo kama hii ambayo ni ya kisiasa huwanyima haki watu
wanaoipenda sanaa hii na walio tayari kujifunza kwa moyo mmoja. Nimeshuhudia
vijana wakitimuliwa mahali fulani ili wasiendelee kujifunza karate kwa hofu za
kisiasa kwamba huenda walikuwa wakijifunza na kumilikiwa na chama fulani cha
siasa kwa sababu za kiulinzi.
Lakini pia kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiogopa kujifunza sanaa hii kwa
hofu ya umri, jinsia, kuvunja viungo, kupoteza maisha n.k.
Kuna wakati ni haki yao kufikiria hivyo kutokana na picha wanayoipata kutoka kwenye
shule mbalimbali zinazoendeshwa na walimu wasio na taaluma ya kutosha
kuhusiana na sanaa hii. Walimu hawa wasio wasomi wa sanaa hutoa mafunzo
potofu ambayo hutoa picha mbaya katika jamii na kusababisha baadhi ya wanafunzi
kukimbia mafunzo.

•UHABA WA MAFUNZO YA KARATE KATIKA MASHULE NA VYUO MBALIMBALI
Japan iliweza kuiendeleza vizuri karate kutokana na sera za kuipeleka katika vyuo,
mashule na taasisi mbalimbali za elimu na utamaduni. Baadhi ya walimu wakuu
wa mashule mbalimbali nchini Tanzania wamekuwa wagumu kushawishika katika
kuifanya karate kama moja ya michezo mashuleni. Hii ingeweza kuwasaidia sana
wanafunzi kinidhamu,kiafya , kitabia na kimtazamo.


BAADHI YA STAILI ZA KARATE

•Shotokan (Prof. Funakoshi Gichin)
•Shotokai (Sensei Shigeru Egami na Sensei Hironishi)-Wanafunzi wa F.Gichin
•Goju-Ryu (Sensei Kanryo Higaonna)- Mwanafunzi mwenza wa F.Gichin
•Shito-Ryu (Sensei Mabuni Kenwa)-Mwanafunzi mwenza wa F.Gichin
•Wado-Ryu (Sensei Otsuka Hironori)- Mwanafunzi wa F. Gichin
•Kyokushinkai ( Sensei Masutatsu Oyama)-Mwanafunzi wa F. Gichin

WAASISI WA STAILI MBALIMBALI ZA KARATE

Profesa Gichin Funakoshi

(SHOTOKAN)


Sensei Mabuni Kenwa

(SHITO RYU)




Sensei Higaonna Kanryo

(GOJU RYU)



Sensei Otsuka Hironori

(WADO RYU)


Sensei Masutatsu Oyama

(KYOKUSHINKAI)


Sensei Shigeru Egami na Sensei Hironishi

(SHOTOKAI)


MISEMO YA KUKUMBUKWA KUTOKA KWA
MWALIMU MASHUHURI WA KARATE

Kama kioo kiwezacho kutoa taswira safi pasipo bugudha, au bonde lililo kimya liwezalo kutoa mwangwi,ndivyo mtu anayejifunza karate-do apaswavyo kuwa mbali na fikra za uovu au ubinafsi na kuwa mwenye fikra safi yenye kujitambua, inayoakisi kile inacho kipokea kikamilifu.
Master Gichin Funakoshi
"Karate-do Kyohan"


Karate-Do si swala la kumjuza mtu mbinu za kujihami peke yake bali ni pamoja
na kumudu namna ya kuwa mtu mwenye tabia nzuri na mnyenyekevu katika
jamii .
Master Gichin Funakoshi
"My Way of Life"



SHULE YA SHOTOKAN KARATE ILIYOPO MWENGE (2008)



Sensei Kolowa .P. Chikoko(mbele) akitoa mafunzo,mstari wa kwanza kutoka kushoto ni Majaliwa na katikati ni Caesar(Mhariri wa blog hii)

INDIA 2009



Kushoto ni Caesar akiwa na Sensei Subramanian K.V


INDIA(Bangalore), 2009



Caesar wa pili kutoka kulia (waliosimama), wa tatu ni Sensei Subramanian.