Pages

Monday, May 24, 2010

KANCHO HIROKAZU KANAZAWA (10TH DAN)

Kancho H.Kanazawa ni moja kati ya walimu wakubwa wa sanaa ya mapigano walio hai.
Ni moja kati ya walimu wachache waliofundishwa na O'Sensei Funakoshi Gichin katika
enzi za uhai wake.

Kanazawa Sensei alizaliwa mwaka 1931 huko Japani, na kama makarateka walio wengi wa
enzi hizo, alianza sanaa ya mapigano kwa kujifunza Judo. Wakati alipokuwa akisoma
katika chuo kikuu cha Takushoku, ndipo alipoanza mafunzo ya Karate chini ya M.Nakayama
aliyekuwa mwalimu mkuu wa Japan Karate Association (JKA).

Huko Japani H.Kanazawa alichukua umaarufu mnamo mwaka 1957 alipokuwa akishiriki
mashindano ya taifa(All Japan Karate Championship) na kuibuka mshindi katika mechi
zote akiwa amevunjika mkono na kukiuka ushauri wa daktari. Mama yake alikuwa moja ya
washabiki kwenye jukwaa na inasemekana kwasababu hiyo, Kanazawa hakutaka 'kumuangusha'.
Kilikuwa ni kitu cha ajabu kwasababu watu aliokabiliana nao walikuwa si wakuingilika
hata unapokuwa na silaha.

Baada ya kumaliza programu ya ualimu ya JKA, Kanazawa akapangiwa kwenda kufundisha
Hawaii, baada ya miaka mitano, mnamo mwaka 1966, akapelekwa Uingereza ambako alipata
dani ya sita ya Shotokan Karate kutoka kwa walimu wakuu wa JKA.

Uungwana, ucheshi na unyenyekevu wake uliwashangaza wengi kutokana na mamlaka pamoja
na heshima aliyokuwa nayo. Mnamo mwaka 1967 aliteuliwa kuwa mwalimu mkuu wa JKA katika
bara la ulaya.

Hatahivyo, mnamo mwaka 1977, Kanazawa akiwa na dani saba alilazimishwa kuondoka JKA
kutokana na sababu za kiofisi. Watu wengi wakajua kwamba ulikuwa ni mwisho wa malengo
na safari yake katika sanaa ya mapigano. Ndipo alipoanzisha Shotokan Karate International
Federation (SKIF). Shirikisho lenye zaidi ya wanafunzi 2,000,000 hivi leo, Tanzania
ikiwa ni moja ya nchi wanachama chini ya uongozi wa Sensei Kolowa.P.Chikoko. Hiyo idadi
'inawafunga mdomo' watu wengi ambao hawakumtakia mema.

Ukiachiliambali mafanikio yake kishirikisho, lakini pia Kancho Kanazawa ameandika vitabu
vingi vya Karate na muongozo wa kiroho kwa ujumla ambavyo vimenunuliwa kwa wingi mno dunia
nzima. Kanazawa kama Funakoshi na Nakayama ni mtu anayeendelea 'kuumiza kichwa' katika
kuiboresha sanaa hii tukufu ya mapigano.

No comments:

Post a Comment