Pages

Sunday, March 28, 2010

TOFAUTI BAINA YA KARATE NA KUNG-FU

Ni kawaida kwa watu wengi wasio jifunza sanaa za mapigano na hata baadhi wanafunzi wa sanaa
hizi kujiuliza juu ya tofauti baina ya karate na kung-fu.
(Kwa wale watakaotaka kujua historia ya kuzaliwa kwa karate kwa ufupi, naomba warejee kwenye
makala zangu za januari 2010)

Kimsingi karate sambamba na staili nyingi za sanaa ya mapigano imezaliwa kutoka kwenye
kungu-fu. Karate imeundwa na kuwekwa katika mfumo ambao mtu yeyote ataweza kujifunza
na kuwa mkufunzi pasipo kujali umri, jinsia, nguvu au umbo la msanii. Tofauti na karate,
kung-fu kwa ujumla haipo kwenye mfumo ambao kila mtu ataweza kujifunza kiurahisi. Kuna
staili nyingi za kung-fu ambazo hutegemea sana umri wa mtu anayetaka kujifunza, nguvu yake,
ulaini wa viungo, wepesi, jinsia n.k.

Ijapokuwa mtu anayetaka kujifunza kung-fu anaweza akatafuta staili inayo endana na umbile
lake au jinsia aliyonayo lakini anaweza kushindwa kujifunza staili iliyompendeza na
bado atakuwa katika wakati mgumu kwasababu bado mifumo ya kung-fu iko mingi mno na hiyo
ni pamoja na ugumu wa kupata mwalimu anayefundisha mfumo atakaoutaka. Karate ina staili chache
mno ukilinganisha na kung-fu, na hii inarahisha upatikanaji wa staili ya msanii popote aendapo.

Hivyo tunaona ni jinsi gani ambavyo kung-fu ina kaubaguzi fulani tofauti na staili nyingi
za karate. Lakini hii si kusema kwamba karate ni rahisi na kung-fu ni ngumu au kinyume chake,la, kiufundi hakuna staili ya sanaa za mapigano iliyo bora au rahisi kuliko nyingine.
Inategemea na yule msanii wa ile sanaa kwamba anaiwakilisha vipi sanaa yake mbele ya hadhira.

Msanii wa karate anaweza kuionyesha sanaa yake mbele ya hadhira na kuzikonga nyoyo za
watazamaji kuliko msanii wa kung-fu, au msanii wa kung-fu kuwapendeza watu kuliko wa karate.
Hii yote itategemea na msanii. Hiyo ni kusema kwamba hakuna staili mbovu bali kuna wasanii wabovu. Na tena hakuna mwanafunzi mbovu ila kuna walimu wabovu. Tukimuangalia mwanafunzi
tunapata taswira kwamba mwalimu atakuwaje pasipo kujali kipaji cha mwanafunzi.

Kitaalam, mbinu nyingi za kung-fu zipo katika mifumo ya mduara(circular) wakati mbinu nyingi
za karate zipo katika mifumo minyoofu(linear).

Katika karate, kwa madaraja ya awali, viwango hutofautishwa na rangi za mikanda mpaka pale
karateka atakapofikia mkanda mweusi tayari kuendelea na madaraja ya mkanda mweusi. Wasanii wa
kung-fu kwa kawaida huwa hawana mifumo ya rangi za mikanda n.k. Kuna wakati hutofautisha
viwango vya wasanii kwa kutumia rangi za mavazi ya mazoezi.

Staili nyingi za karate huchezwa peku (kwa watakaotaka kujua sababu naomba warejee kwenye makala
yangu ya kwanza ya mwezi huu), wakati saili nyingi za kung-fu huchezwa na viatu.

Katika karate, kwa kawaida matumizi ya silaha hufundishwa katika madaraja ya juu(mpaka msanii atakapoweza
kujimudu vyema pasipo utegemezi wa silaha) tofauti na kung-fu ambapo wasanii wengi hutumia
muda wao wote wa mafunzo kujifunza au kufundishwa namna ya kuzimudu baadhi ya silaha za mapigano.

Nimejitahidi kuelezea tofauti baina ya karate na kung-fu kwa kadri ya uwezo wangu, ni matumaini
yangu itawawia rahisi kujaribu kutafautisha baina ya hizi staili mbili za mapigano. Tofauti ya
haraka-haraka ni kwamba maranyingi(na si wakati wote) karateka huwa kwenye mavazi meupe,peku na
kiwango hutegemea mkanda aliouvaa wakati wa kung-fu huweza kuwa kwenye mavazi yenye rangi mbalimbali
kama orenji, njano, bluu, nyeusi n.k, akiwa amevaa viatu na vitambaa vya mavazi yao huwa laini.

MSANII WA KARATE(SENSEI GEORGE BEST).

WASANII WA KUNG-FU.

No comments:

Post a Comment