Pages
▼
Saturday, January 9, 2010
MUHTASARI WA MASHINDANO YA KATA ITALY
MAANA YA KATA KATIKA KARATE
Kata ni makabiliano ya kufikirika baina ya karateka na wapinzani kutoka pande mbalimbali.
Tunatumia neno wapinzani badala ya maadui kwa sababu kwenye falsafa za karate hatuna adui.
Kila staili ya karate ina kata zake ijapokuwa baadhi zinafanana kiustadi, majina n.k.
Vipengele vitatu muhimu ambavyo karateka anapaswa kuvizingatia pindi aichezapo kata:
i)Nidhamu katika matumizi ya nguvu. Nguvu kuu inapaswa kutumika katika ile sekunde
ya shambulizi tu, baada ya shambulizi karateka atatakiwa kutoka katika hali ya ukakamavu
ili kuepuka uzalishaji wa nguvu isiyo na matumizi na hatimaye kupoteza nguvu bila sababu.
Lakini kuna kata kama hangetsu au kata nyingi za gojyu-ryu ambazo humtaka karateka
kukakamaa kuanzia mwanzo wa kata mpaka mwisho. Hapo kipengele cha kwanza si lazima
kipewe kipaumbele.
ii)Udhibiti wa spidi ya mbinu. Karateka anapaswa kutambua vyema ni mbinu gani katika kata
zinapaswa kufanywa taratibu na zipi atatakiwa kuzifanya haraka iwezekanavyo, hii pia hutumika
katika kuijua spidi ya karateka. Kama ilivyo kwa mwanamichezo au msanii, karateka anatakiwa
audhibiti mwili wake na si mwili umdhibiti yeye.
iii)Mikao na hatua sahihi pamoja na upumuaji.
Mikao na hatua katika kata ni lazima viwe sahihi ili kutoa tafsiri sahihi ya kata. Lakini pia namna
ya upumuaji ni kitu muhimu mno hasa katika viwango vya juu sana kwenye karate. Kuna wakati
upumuaji hupewa kipaumbele kuliko mbinu ya karate kwa sababu pumzi ni uhai. Upumuaji
mzuri utamsaidia sana karateka katika matumizi ya nguvu na kumfanya aweze kudumu kwenye
zoezi au pambano kwa muda mrefu.
Hivyo ni vipengele muhimu sana katika kata, vipengele vingine muhimu ni kama ; uzatiti wa wazo katika mbinu, mtikiso wa kiuno, kutanuka na kusinyaa kwa mwili na hatua, uelekeo, mlio wa shambulizi(kiai ), nidhamu, shabaha ya mbinu, stemina, muda, kujiamini, morali, tahadhari (zashin) na kadhalika.
No comments:
Post a Comment