Sunday, March 28, 2010

TOFAUTI BAINA YA KARATE NA KUNG-FU

Ni kawaida kwa watu wengi wasio jifunza sanaa za mapigano na hata baadhi wanafunzi wa sanaa
hizi kujiuliza juu ya tofauti baina ya karate na kung-fu.
(Kwa wale watakaotaka kujua historia ya kuzaliwa kwa karate kwa ufupi, naomba warejee kwenye
makala zangu za januari 2010)

Kimsingi karate sambamba na staili nyingi za sanaa ya mapigano imezaliwa kutoka kwenye
kungu-fu. Karate imeundwa na kuwekwa katika mfumo ambao mtu yeyote ataweza kujifunza
na kuwa mkufunzi pasipo kujali umri, jinsia, nguvu au umbo la msanii. Tofauti na karate,
kung-fu kwa ujumla haipo kwenye mfumo ambao kila mtu ataweza kujifunza kiurahisi. Kuna
staili nyingi za kung-fu ambazo hutegemea sana umri wa mtu anayetaka kujifunza, nguvu yake,
ulaini wa viungo, wepesi, jinsia n.k.

Ijapokuwa mtu anayetaka kujifunza kung-fu anaweza akatafuta staili inayo endana na umbile
lake au jinsia aliyonayo lakini anaweza kushindwa kujifunza staili iliyompendeza na
bado atakuwa katika wakati mgumu kwasababu bado mifumo ya kung-fu iko mingi mno na hiyo
ni pamoja na ugumu wa kupata mwalimu anayefundisha mfumo atakaoutaka. Karate ina staili chache
mno ukilinganisha na kung-fu, na hii inarahisha upatikanaji wa staili ya msanii popote aendapo.

Hivyo tunaona ni jinsi gani ambavyo kung-fu ina kaubaguzi fulani tofauti na staili nyingi
za karate. Lakini hii si kusema kwamba karate ni rahisi na kung-fu ni ngumu au kinyume chake,la, kiufundi hakuna staili ya sanaa za mapigano iliyo bora au rahisi kuliko nyingine.
Inategemea na yule msanii wa ile sanaa kwamba anaiwakilisha vipi sanaa yake mbele ya hadhira.

Msanii wa karate anaweza kuionyesha sanaa yake mbele ya hadhira na kuzikonga nyoyo za
watazamaji kuliko msanii wa kung-fu, au msanii wa kung-fu kuwapendeza watu kuliko wa karate.
Hii yote itategemea na msanii. Hiyo ni kusema kwamba hakuna staili mbovu bali kuna wasanii wabovu. Na tena hakuna mwanafunzi mbovu ila kuna walimu wabovu. Tukimuangalia mwanafunzi
tunapata taswira kwamba mwalimu atakuwaje pasipo kujali kipaji cha mwanafunzi.

Kitaalam, mbinu nyingi za kung-fu zipo katika mifumo ya mduara(circular) wakati mbinu nyingi
za karate zipo katika mifumo minyoofu(linear).

Katika karate, kwa madaraja ya awali, viwango hutofautishwa na rangi za mikanda mpaka pale
karateka atakapofikia mkanda mweusi tayari kuendelea na madaraja ya mkanda mweusi. Wasanii wa
kung-fu kwa kawaida huwa hawana mifumo ya rangi za mikanda n.k. Kuna wakati hutofautisha
viwango vya wasanii kwa kutumia rangi za mavazi ya mazoezi.

Staili nyingi za karate huchezwa peku (kwa watakaotaka kujua sababu naomba warejee kwenye makala
yangu ya kwanza ya mwezi huu), wakati saili nyingi za kung-fu huchezwa na viatu.

Katika karate, kwa kawaida matumizi ya silaha hufundishwa katika madaraja ya juu(mpaka msanii atakapoweza
kujimudu vyema pasipo utegemezi wa silaha) tofauti na kung-fu ambapo wasanii wengi hutumia
muda wao wote wa mafunzo kujifunza au kufundishwa namna ya kuzimudu baadhi ya silaha za mapigano.

Nimejitahidi kuelezea tofauti baina ya karate na kung-fu kwa kadri ya uwezo wangu, ni matumaini
yangu itawawia rahisi kujaribu kutafautisha baina ya hizi staili mbili za mapigano. Tofauti ya
haraka-haraka ni kwamba maranyingi(na si wakati wote) karateka huwa kwenye mavazi meupe,peku na
kiwango hutegemea mkanda aliouvaa wakati wa kung-fu huweza kuwa kwenye mavazi yenye rangi mbalimbali
kama orenji, njano, bluu, nyeusi n.k, akiwa amevaa viatu na vitambaa vya mavazi yao huwa laini.

MSANII WA KARATE(SENSEI GEORGE BEST).

WASANII WA KUNG-FU.

Sunday, March 14, 2010

MSIBA

KWANIABA YA MAKARATEKA WENZANGU, NAPENDA KUTOA POLE KWA KARATEKA MWENZETU
SWALEHE MWATIKA (BLACK BELT) WA MLALAKUWA KWA KUFIWA NA BABA YAKE MZAZI.
SISI TULIMPENDA LAKINI MUNGU ALIMPENDA ZAIDI, MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA
MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI AMINA.

Friday, March 12, 2010

BAADHI YA MITINDO ITUMIKAYO KATIKA KUMITE

1)Kake no sen

Mpinzani wako amekwisha kusudia kuja na shambulizi na
amekwisha ingia kwenye ngome yako, pasipo kukinga
unamuwahi na pigo(haraka sana) kabla hajamaliza shambulizi lake.

2)Tai no sen(Sen no sen)

Wakati mpinzani wako anaanza kuvurumisha pigo lake,
unambabatiza na kinga(kabla hajamaliza shambulizi),
na kumuwahi yeye papo hapo.

3)Go no sen

Mpinzani wako amekwisha shambulia, umekwisha kinga au umemkwepa
na kuanza kurudisha mashambulizi kwenye nafasi zitakazo patikana.
Hapa unamruhusu amalize mashambulizi yake kisha unaanza wewe.


Aina ipi ni nzuri kutumia itategemea na mpiganaji kwani
wapiganaji wengi hutofautiana katika matumizi ya hizi mbinu.

Tuesday, March 2, 2010

MWALIMU MZURI ANATAKIWA AWE NA VIGEZO GANI?

1. Kuipenda sanaa au taaluma yako( unayofundisha).

2. Kuelewa kikamilifu manufaa na umuhimu wa taaluma yako kiujumla.

3. Kuwa na tabia ya kujumuika na wataalamu(waalimu) mbalimbali pale upatapo nafasi.

4. Kujua namna ya kukabiliana na vipingamizi vinavyo zuia malengo yako pamoja na yale ya wanafunzi wako.

5. Jaribu kuwafundisha wanafunzi wako ili waje kuwa bora kuliko wewe.

6. Wakati wote endelea kujifunza na kuyaishi yale unayofundisha ili uwe dira kwa wengine.

7. Ni vizuri na muhimu kuwaelewa wanafunzi wako kisaikolojia(tabia zao kwa ujumla).

8. Wapongeze wanafunzi pale wanapostahili pongezi.

9. "Fundisha yale mwanafunzi anayopaswa kujifunza"- Sensei Jean Claude Van Damme

10. "Siku zote kumbuka fikra na makusudio yako wakati ulipokuwa ukianza mafunzo"- Meijin Funakoshi G.

Friday, February 19, 2010

FALSAFA ZA O'SENSEI

MIONGOZO 22 YA MEIJIN GICHIN FUNAKOSHI

1. Karate huanza na kumalizika kwa nidhamu.
2. Daima fikiri kiubunifu.
3. Fikra huja kabla ya mwili.
4. Jiweke tayari kuwa huru kifikra.
5. Jitambue kwanza ndio uwatambue wengine.
6. Karate ni muongozo wa haki na inapaswa kutumika hivyo tu.
7. Sogea kufuatana na mpinzani wako.
8. Kamae ni kwa wanafunzi wapya na shizentai ni kwa wazoefu.
9. Usifikirie kwamba inabidi ushinde ila fikiri kwamba hupaswi kushindwa.
10. Karate si katika Dojo peke yake.
11. Husisha karate katika kila jambo ulifanyalo, wakati wote fikiri kuitumia miongozo hii kila siku.
12. Mafunzo ya karate ni ya wakati wote wa maisha yako.
13. Karate ni kama maji ya moto, yasipoendelea kupashwa moto au kuhifadhiwa na joto lake, hupoa.
14. Mara tu utokapo nyumbani, una wapinzani zaidi ya elfu moja.
15. Hakuna shambulio la kwanza kwenye karate.
16. Elewa tofauti ya sehemu zenye madhara na zisizo na madhara.
17. Uzembe huja kabla ya ajali.
18. Fikiri mikono na miguu yako kuwa kama sime.
19. Kumbuka vipengele vigumu na vyepesi kwenye kata.
20. Karate ikifanyika vyema ni tofauti na kombati(struggle fighting).
21. Jihadhari na matendo yako, usije ingia matatani.
22. Mafunzo ya kata si uhalisi wa jambo lenyewe.

Friday, February 5, 2010

THE ' BLACK PEARL '

NINI MAANA YA KUMITE ?

Sehemu nyingine ya mafunzo ya karate hujumuisha makabiliano baina ya wanafunzi, hii kwa neno
la kijapani huitwa kumite. Kumite hufundishwa kwa hatua mbalimbali kutegemea na staili ya karate.

Kimsingi wanafunzi hujifunza ustadi sahihi wa kushambulia na kuyakabili mashambulizi katika mikanda
ya awali kabla ya kuruhusiwa kukabiliana wakiwa huru kushambulia na kujikinga na mashambulizi.

Lakini watu wengi hapa nchini hufundisha kinyume na taratibu hizi za kitaalam.
Mbaya zaidi wanafunzi hufundishwa kushambulia pasipo na tahadhari.
Mashambulizi ya karate ni lazima yadhibitiwe na yule anayeshambulia
ili kuondoa hatari kama kifo, kuvunjika n.k. Kuna baadhi ya wakufunzi wa karate ambao wana uwezo
mkubwa wa kutoa uhai wa mtu kwa pigo moja tu. Watu wa namna hii wanaelewa hatari iliyopo katika
kumite na siku zote hudhibiti mashambulizi yao kuepusha hizo hatari ikiwa ni pamoja na kuifanya
karate kama sanaa ambayo mtu yeyote ataweza kujifunza pasipo kujali jinsia, umri, umbo au nguvu
aliyonayo.

Tukirudi kwenye falsafa ya karate kumite niliyo izungumzia hapo juu ni 20% ya kumite halisi
katika karate. Asilimia themanini iliyobaki ni mapigano baina na wewe na madhaifu yako . Hii ndiyo
kumite ya kweli inayo kamilisha maana ya karate-do. Kila mtu ni mdhaifu wa jambo fulani, laweza
kuwa moja au zaidi. Hivyo basi ni vema tukaishi tukiyapunguza madhaifu yetu katika safari ya maisha
yetu.



MSIBA WA KARATEKA SAMSON MWAMANDA

Tunasikitika kutangaza kifo cha karateka mwenzetu, Samson Mwamanda (green belt) aliyefariki
dunia ghafla usiku wa kuamkia tarehe 27/01/2010 baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Ijapokuwa sisi tulimpenda sana lakini Mungu alimpenda zaidi.
Tunatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki wa marehemu.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
Amina



Pichani mdogo wetu Samson Mwamanda wa kwanza kutoka kulia(walio kaa)